Monday, May 31, 2010

MZEE PWAGU AZIKWA


Mzee Pwagu, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 88, kwenye Hospitali ya Amana, Ilala majira ya saa 10 alasiri na kuzikiwa siku iliyofuata kwenye makaburi ya Kigogo CCM, Dar.
Ijumaa Wikienda lilikuwepo wakati wa mazishi na kushuhudia umma wa watu waliojitokeza kwa wingi kumsindikiza mzee Pwagu kwenye safari ya dawamu.

Wasanii wengi walifika kwenye mazishi hayo ambapo walieleza kusikitishwa kwao.
Walisema kuwa mzee Pwagu alikuwa mlezi wa wasanii wengi hasa wa maigizo na kwamba muongozo wake umesaidia kuwaweka kwenye ramani.
Katibu wa Kundi la Kaole Sanaa, Simon Simalenga ‘Mr. Dimera’ alisema kuwa Pwagu ni mwenyekiti muasisi wa kundi hilo ambalo lilianzishwa mwaka 1998.

“Alishirikiana na watu sita, akiwemo Mama Haambiliki, Cristant Mhenga, Chuma Suleiman ‘Bi. Hindu’, Fatuma Rajabu ‘Bi. Kidide’ na Said Fundi ‘Mzee Kipara,” alisema Mr. Dimera.
Kwetu sisi, Pwagu alikuwa shujaa kwa sababu jitihada zake, uvumilivu na kujitolea ndivyo vimewezesha sanaa ya maigizo kukubalika Tanzania, kukua na kuzaa soko la filamu.

Iliandikwa kwamba lazima watu wengine watengeneze barabara halafu wengine wapite, Mzee Pwagu atabaki kukumbukwa kwa ujenzi wake wa sanaa ambao unawezesha ajira ya vijana wengi hivi sasa.
Mungu ni sababu ya kila kitu.
Inna Lillah Wainna Ilayh Rrajiuun.

No comments:

Post a Comment