Thursday, February 17, 2011

WAKUSWAMPA KITAA



Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imewataka Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dr. Hussein Mwinyi na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange kujiuzulu mara moja ili kuwajibika kisiasa kutokana na maafa ya Gongo la Mboto na ili kupisha uchunguzi huru na wa kina wa chanzo na/au sababu za milipuko hiyo. Mh. Selasini alisema: “Dr. Hussein Mwinyi alikuwa Waziri wa Ulinzi wakati wa maafa ya Mbagala; na Jenerali Mwamunyange alikuwa Mkuu wa Majeshi. Maafa ya Mbagala yalitokea chini ya dhamana na/au usimamizi wao. Na mara baada ya maafa hayo, Waziri Mwinyi na Jenerali Mwamunyange waliliahidi taifa kwamba maafa ya aina hii hayatatokea tena. Sasa yametokea. Inaelekea, kwa hiyo, kwamba ahadi yao ilikuwa sio ya kweli na/au hawakuhakikisha kwamba inafanyiwa kazi ili iwe ya kweli. Viongozi hawa hawana budi kuwajibika kwa hiari yao wenyewe au kuwajibishwa kama itahitajika.”

Mh. Selasini aliongeza kusema kwamba hadi leo hakuna taarifa yoyote rasmi iliyowahi kutolewa hadharani kwa wananchi na/au kwa wawakilishi wao Bungeni ya chanzo na/au sababu za maafa hayo. “Hadi leo hii wananchi na/au wawakilishi wao Bungeni hawajaambiwa kama kulikuwa na makosa ya makusudi na/au ya uzembe na/au kama hatua zozote za kinidhamu na/au za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya mtu yeyote kutokana na kusababisha na/au kuwajibika kwa maafa hayo. Jana maafa mengine ya aina hiyo hiyo yametokea tena na kwa kadri ya taarifa rasmi ya Serikali watu wengi wameuawa na wengi wengine kujeruhiwa na mali nyingi kuharibiwa. Kwa sababu hizo, huu ni wakati muafaka kwa Dr. Mwinyi na Jenerali Mwamunyange kuonyesha uadilifu wao kwa kujiuzulu nafasi zao ili kuwajibika kwa maafa haya.”

Mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imependekeza iundwe Tume Huru ya Uchunguzi na/au Kamati Teule ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuchunguza kwa kina chanzo, sababu na madhara yote yaliyosababishwa na milipuko ya Gongo la Mboto. “Kwa kuzingatia historia ya uchunguzi wa milipuko iliyotokea Mbagala mwezi Aprili 2009, Tume Huru na/au Kamati Teule ya Bunge lazima itoe taarifa yake hadharani kwa kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, alishauri Mh. Selasini.
MAONI YANGU:Kila jambo na wakati wake lakini kwa ushauri wangu kuna haja ya kuwashirikisha wazee wastaafu wa liokuwa jeshini waje kuangalia ni kwa nini hali hii inajitokeza sana kwa wakati huu labda kuna mapungufu katika uhifadhi wa hayo mabomu,kamanda liangalie hilo kwa umakini.

No comments:

Post a Comment