Wednesday, April 20, 2011

40 YA 5 STARS




Machozi, simanzi na huzuni vimeibuka upya wakati wa kuhitimisha siku 40 za msiba wa vifo vya wanamuziki 13 wa Kundi la Five Stars Modern Taarab waliopoteza maisha kwa ajali ya gari huko Mikumi, Morogoro usiku wa Jumatatu ya Machi 21, mwaka huu.

Tukio hilo la hitma lililoshuhudiwa na gazeti hili lilijiri katika Ukumbi wa PTA Sabasaba, Temeke jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita ambapo lilihudhuriwa na kadamnasi kutoka sehemu mbalimbali, nje na ndani ya jiji.
baadhi ya wanamuziki walionusurika kwenye ajali hiyo wakitokwa na machozi hivyo kuibua upya vilio kwa mastaa na watu wengine waliokuwa wakiwakumbuka marehemu kifamilia na kimuziki.


“Unajua watu wakikumbuka ajali yenyewe ilivyokuwa, lazima watokwe machozi,” alisema mmoja wa wakurugenzi wa kundi hilo, Ferouz Juma na kuongeza:
“Kwa sasa ni vigumu kufikiria kurudi upya kwa kundi letu kwani wengi wetu tuna vitu vinatusumbua vichwani.

“Bado wanamuziki wetu walionusurika wanahitaji muda wa ziada kulitafakari lile tukio.
“Kila mmoja akimtazama mwenzake hapa anatokwa na machozi hasa wakivuta hisia kwa wenzao waliopoteza maisha wakiwa wanawaona.”

ZENA ATANGAZA KUACHA MUZIKI

Mwimbaji mkongwe wa kundi hilo aliyedumu katika muziki wa mwambao kwa zaidi ya miaka kumi, Zena Mohamed ambaye alinusurika kifo kwenye ajali hiyo alilieleza gazeti hili kuwa, amepoteza imani na muziki hivyo hafikirii kurejea tena jukwaani.
Alitoa kilio chake kuwa, tangu lilipotokea tukio hilo na yeye kuponea chupuchupu, amekuwa akisumbuliwa na ndoto za ajabu ajabu kila kukicha.
Alifunguka: “(Huku akitokwa machozi) Nahisi kama Israel mtoa roho za watu ananifuata kila ninapokwenda.
“Achilia mbali kupanda jukwaani ambako sitaki kusikia, lakini hata nikiwa nyumbani hali ya maruweruwe huwa inanijia mara kwa mara kichwani

MAREHEMU
Katika ajali hiyo waliopoteza maisha ni pamoja na Issa Ally ‘Kijoti’, Husna Mapande, Sheba Juma ‘Jasusi’, Omary Hashim na Hamisa Mussa.
Wengine ni Ramadhan Maheza ‘Kinyoya’, Omary Tall, Samir Maulid, Hajji Mdahaniwa, Hassan Ngereza, Maimuna Makuka ‘Kisosi’, Hajji Babu na Tizo Mgunda.

No comments:

Post a Comment